Wednesday, May 11, 2011

Nipo tayari kunyanganywa kadi- Moyo


MUASISI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mzee Hassan Nassor Moyo amesema yuko tayari kurejesha kadi ya chama chake iwapo atalazimika kufanya hivyo huku akisisitiza kuunga mkono Muungano wa Mkataba.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Zanzibar Moyo amesema ataendelea kuutetea msimamo wake wa kutaka Muungano wa mkataba kwa kuwa muungano uliopo kw
a miaka 48 sasa umeshindwa kutatua kero zilizopo na kuleta matumaoni kwa wazanzibari.

“Jambo kubwa ni nchi chama lilikuwa jambo la pili na kama viongozi wetu wa chama wanataka kutupeleka huko tukaeleze msimamo wa chama, mimi nasema muungano umekuja kwanza na hivyo ndio ninavyojua mimi na huo ndio msimamo wangu lakini ikiwa wanatwambia turejesha kadi mimi nitakuwa tayari lakini siwezi kuacha nchi yangu …nchi ilikuwa jambo la mwanzo” alisiitiza Mzee Moyo.


Kauli hiyo ya Moyo imekuja siku chache baada ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai kuwataka wafuasi wote wa chama hicho kuheshimu sera ya chama ambayo ni serikali mbili kama ilivyo hivi sasa na kuwaonya wale wote ambao watakwenda kinyume na chama hicho.


Mbali ya kauli ya Vuai, Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mjini kilipitisha azimio la kuwataka baadhi ya wabunge, wawakilishi, Muweka Hazina wa Chama hicho Mansoor Yussuf Himid na Makamo Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar Amani Abeid Karume kuacha tabia ya kuhubiri sera za vyama vyengine.


Azimio hilo lililopitishwa na wajumbe 400 lilisema viongozi hao wamekuwa na tabia ya kuunga mkono msimamo wa kutaka mabadiliko ndani ya muungano msimamo ambao unakwenda kinyume na msimamo wa chama chao ambapo sera za chama cha CCM ni serikali mbili zenye mfumo uliopo ambapo masuala la muungano ni kushughulikiwa na sio kubadili mfumo.


Akitoa historia refu ya harakati zake za ukombozi mbele ya waandishi wa habari, Mzee Moyo alisema anashangazwa na kauli ya kuwanyamazisha wananchi wasitoe maoni yao kwa kisingizio cha kwenda kinyume na sera za CCM wakati suala la Muungano ni muhimu zaidi kuliko chama.


“Chama kimekua baadae kwanza ilianza nchi na ukanja muungano sasa msiwazuwie watu kutoa maoni yao kwa kutwambia chama kinasema hivi au vile” alisema Mzee Moyo huku akionesha uso wa kukasirika.


Akitoa historia refu na nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar Mzee Moyo alisema kwamba viongozi na waasisi wa muungano walikuwa wamekubaliana baadhi ya mambo katika muungano mwaka 1970 baada ya viongozi wa Baraza la Mapinduzi kuhoji uendeshaji wa shughuli za Muungano na kutangaza hatua kadhaa ikiwemo ya kutaka Rais wa Zanzibar kujulishwa juu ya hali ya hatari inapotokea Tanzania.


Akizitaja hatua nyengine zilizokubalika, Moyo alisema Baraza la Mapinduzi lilitaka kila upande wa Muungano ujitegemee kwa kila upande kuwa na jeshi lake la polisi, kuwa na mamlaka kamili juu ya masuala ya uhusiano wa kimataifa na pia pande hizo kila moja kuwa na sarafu yake.


Alisema baada ya viongozi wa Baraza la Mapinduzi wakiwa wamefuatana na Mzee Karume kutoa hoja hiyo mbele ya Mwalimu Nyerere wakaambiwa, muda wa suala hilo haujafika ambapo alisema ikiwa wakati ule haujafika basi sasa ni wakati wake.


“Alipoambiwa Mwalimu Nyerere basi akasema muda haujafika lakini leo vijana nakwambieni kwamba muda umeshafika na muda huu ndio wakati wake wa kuyasema haya msiogope” aliwaambia vijana ambao walialikwa katika mkutano huo wa waandishi wa habari.


Mzee Moyo, aliyewahi kuwa waziri na kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano alisema aliwataka vijana kuendelea kutoa maoni yao bila ya woga kwani kufanya hivyo ni kuendeleza kazi aliyokuwa akiifanya Mzee Karume kutetea nchi yake.


Aidha Mzee Moyo ambaye ni miongoni mwa waasisi wa Mapinduzi na Muungano alisema chanzo cha Zanzibar kuibua madai hayo, yalitolewa baada ya Mwalimu Nyerere kuamuru kikosi cha jeshi kutoka Zanzibar kwenda katika shughuli za vita vya ukombozi wa Msumbiji bila kumwarifu Rais wa Zanzibar jambo ambalo halikumfurahisha Mzee Karume.


Mzee Moyo atakuwa ni mwana CCM wa kwanza kukariri hadharani maneno ya Mzee Karume aliyosema dhidi ya Muungano juu ya mambo iwapo yatakwenda kombo.


“Mzee Karume alisema wazi muungano kama kofi likikukera unalivua lakini pia Mzee Karume aliufananisha huu muungano na kanzu ambapo alisema unaweza kuivua” alisisitiza Mzee Moyo ambaye alisema kutoa maoni ni moja ya uhuru na sera za chama chake.


Aidha Mzee Moyo alikumbushia yaliomkuta Rais wa awamu ya pili ya serikali ya Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi pia hakufanya makosa aliotaka Muungano unaoendeshwa bila kuingilia mambo ya Zanzibar na serikali nyingine inayoshughulikia masuala ya Tanganyika yasiyokuwa ya Muungano lakini akasema bahati mbaya nia hiyo ilikuwa amekwenda nayo peke yake bila ya kuwashauri wenzake.


“Sisi tulikaa kimya kwa sababu yeye kama kiongozi mkuu wa nchi akaona aende nayo peke yake kwa hivyo Moyo akaa kimya hakusema kitu lakini angatwambia sisi tungemuunga mkono” alikumbushia.


Akitoa nasaha zake Mzee Moyo alisema huu sio wakati tena wa Chama Cha Mapinduzi kuwazuwia watu wasitoe maoni yao bali wanatakiwa kuwaachia watoa maoni yao kwa uhuru na uwazi ili kuunda muungano unaokubalika na wenye maslahi kwa nchi zote mbili Tanyanyika na Zanzibar.


Hata hivyo Mzee Moyo aliwakemea sana viongozi wenye mawazo yao na kukataa kupokea mawazo ya wenziwao na kusema kwamba nchi hii sio ya CCM na kila mmoja awe huru kutoa maoni yao na kuwataka viongozi wa CCM wavumilie juu ya maoni yanayotolewa.


“Mimi nasema suala la Muungano haliwezi kugeuzwa la Chama, ….chama kumetoa mchango kwa kuunga mkono uamuzi wa serikali mbili –Tangayika na Zanzibar kuungana, sasa mnapotwambia tunakiuka sera za chama …chama gani? Alaa mnataka kuwaziba watu midomo bwana” alisema Moyo.


Aliwaambia viongozio wa CCM wasioweza kutoa kasoro ndani ya muungano na kukataa kutoa muundo wa muungano wajue kuwa wanajidanganya wenyewe na kuwadanganya wenziwao.


Mzee Moyo alisema huwezi kuendesha Nchi kwa sera ya Chama fulani na kudai kwamba Muungano huu hawendi kwa sera za Chama cha Mapinduzi.


Mzee Moyo alifahamisha kuwa Watanganyika walifika pahala na wao wakadai serikali yao lakini chama cha Mapinduzi kiliwazuia.


“Lakini na wambia watanganyika kuwa muda wao ndio huu umefika na wao wadai taifa lao” alisema Mzee Moyo.


Sambamba na hilo Mzee Moyo alitumia fursa hiyo kwa kujibu mapigo kwa wale wote ambo walimwambia yeye amekuwa msaliti wa Chama cha mapinduzi. Mzee Moyo alisema anachokifanya yeye ni kukubali mabadiliko katika taifa ilikuondoa migogoro isiyo ya lazima kwa vizazi vipya.


Alisema kuna viongozi wengi wanauchoyo na kudai kwamba yeye anachokiangalia ni Hadhi ya Zanzibar Kitaifa na kimataifa.


Akijibu hoja za baadhi ya wana CCM waliosema kwamba yeye sio mwana mapinduzi, Mzee Moyo alisema “Kuna watu ambao wanajifanya ni wana Mapinduzi wajue wanachokizungumza na waelewe mimi ni nani katika Kupigania uhuru wa Nchi hii, kuna watu wanadhani mapinduzi yalitayarishwa na watu wa kumi nne hamna lile lilikuwa ni kundi la mapambano lakini lilitayarishwa na Wazanzibar wote” aliongeza.


“Kuna Mtu anaitwa Ali Ameir mwambieni asema anapozungumza kwa wewe ulipindua elewa kuwa haya yote yalitayarishwa kwa muda usiseme jambo usilolijua” aliongeza Mzee Moyo.


Alisema Mzee Karume alimuamini sana na sehemu nyingi alikuwa akimsogeza yeye na kutaka ushauri kwake na kuhoji kwani wakati huo hakukuwa na vijana ambao angeweza kumsaidia Mzee Karume.


“Mimi nikawa championi wa ASP hapa Zanzibar baada ya hapo nikaenda urusi ambapo vyama vilikwenda kuzungumzia uhuru wa Zanzibar na huko nikapiguwa simu niende London mimi nilikuwa observer wa Kwanza na hayo yote ni Mzee Karume alitaka iwe hivyo sasa wajiulize why mimi wasiwe wengine” alihoji Mzee Karume.

No comments:

Post a Comment